| Article Index |
|---|
| Culture Music Club in Darmstadt |
| Page 2 |
| Page 3 |
| Page 4 |
| Page 5 |
| All Pages |
This is a description of the superb Taarab performance exhibited in Darmstadt Germany, by Culture Music Club, a legendary Taarab group from Zanzibar Tanzania. The authors depict the rich and scintillating performance well thought out and choreographed for the fulfilment of the audience. They conclude with the observation that Taarab, in its quest for unity in diversity, continues to play a crucial role in today’s globalising world.
The article is written in Swahili.
Ilikuwa jioni ambayo wengi hawakutarajia, jioni ya tamaduni ya muziki wa mwambao kuweza kuonyeshwa katika mji wa Darmstadt nchini Ujerumani. Wanamuziki wa bendi ya Taarab inayojulikana kama Culture Music Club, Jumamosi ya tarehe 3.11.2007 waliweza kuwafurahisha wananchi wa Ujerumani na wengine toka mataifa mbali mbali, kwa muziki wao wenye ubora na upeo wa kiwango cha juu. Muziki uliweza kuchezwa kwa takribani saa mbili na nusu lakini mwishowe ikaonekana ni kama muda huo ulikuwa wa nusu saa pekee. Nyuso za watazamaji ziling’ara kwa furaha tele huku zile za waafrika ambao walikuwa wanaelewa kiswahili zikabaki meno nje kwa kucheka na kutafakari maneno yaliyokuwa yanaimbwa.
Tulifika pale karibu dakika thelathini kabla ya kuanza kwa onyesho. Jamaa walikuwa wanang’ang’ania tikiti ili wamudu kuwaona hawa wana Culture Music Club kutoka Tanzania ambao wamesifika dunia nzima kwa muziki wao uliochangamka na uzoefu mkubwa ambao unaunganisha bara Asia, Afrika na tamaduni za uarabuni. Mbali na Afrika, sifa zao nyingi hasa zajulikana Ulaya ambako wameweza kutembelea nchi nyingi mara kwa mara wakitumbuiza kwa muziki wao. Kikundi hiki kimerekodi kazi zake nyingi Ulaya. Ingawa watu wa bara la ulaya wamepata kununua kazi zao, na kuwaona mara kadhaa jukwaani, ni vigumu kwa mtu kujizuia kuwaona tena na tena kwani maonyesho yao hayaishi hamu. Kwetu sisi, hii ilikuwa mara yetu ya kwanza kujumuika na watu wa ulaya kwenye onyesho hili la muziki ambapo uliwakilisha tamaduni ya mwambao vizuri.
Wakati tunaingia kwenye ukumbi wa Centralstation dakika chache kabla ya kuanza kwa onyesho, watu tayari walikuwa wametapakaa kote huku wakiongeleshana na kujuliana hali huku wakijituliza kwa vinywaji. Jukwaa lilikuwa limejaa vipaza sauti tofauti tofauti ili kuwezesha sauti kusikika vizuri katika ukumbi wote. Lakini hakukuwa na ala hata moja ya muziki jukwaani.
Punde, taa zikapunguzwa huku nyingine zikizimwa kabisa na kuacha mwangaza katika jukwaa peke yake, hali iliyoonyesha kwamba wakati ulikuwa umewadia. Watazamaji wakaharakisha kutafuta mahali pa kukaa huku wengine wakiandaa kamera ili kuchukua picha. Mara tukasikia makofi ya kushangilia huku wenye vyombo vya kuchukuwa picha wakitafuta nafasi bora ya kupiga picha za wanamuziki. Wasanii wakajipanga kwenye jukwaa huku kila mmoja ameshikilia ala yake ya muziki. Mbele ya jukwaa walijipanga wanaume ambao walivalia kanzu nyeupe na kofia za watu wa mwambao huku wakiongeza na koti jeusi juu. Wanawake waliojipanga kwa kukaa katika mstari wa nyuma nao walikuwa wavalia mavazi yao ya kupendeza ya hariri iliyong’ara kwa kumulikwa na taa. Kwa mavazi yao na mpangilio wao, hawa wana Culture Music Club waashiria uvaaji unaopendelewa na watu wa mwambao. Kwa ujumla kulikuwa na wanawake watatu, wawili wanaimba solo na mmoja wao ambaye alicheza dufu.
