| Article Index |
|---|
| Culture Music Club in Darmstadt |
| Page 2 |
| Page 3 |
| Page 4 |
| Page 5 |
| All Pages |
This is a description of the superb Taarab performance exhibited in Darmstadt Germany, by Culture Music Club, a legendary Taarab group from Zanzibar Tanzania. The authors depict the rich and scintillating performance well thought out and choreographed for the fulfilment of the audience. They conclude with the observation that Taarab, in its quest for unity in diversity, continues to play a crucial role in today’s globalising world.
The article is written in Swahili.
Ilikuwa jioni ambayo wengi hawakutarajia, jioni ya tamaduni ya muziki wa mwambao kuweza kuonyeshwa katika mji wa Darmstadt nchini Ujerumani. Wanamuziki wa bendi ya Taarab inayojulikana kama Culture Music Club, Jumamosi ya tarehe 3.11.2007 waliweza kuwafurahisha wananchi wa Ujerumani na wengine toka mataifa mbali mbali, kwa muziki wao wenye ubora na upeo wa kiwango cha juu. Muziki uliweza kuchezwa kwa takribani saa mbili na nusu lakini mwishowe ikaonekana ni kama muda huo ulikuwa wa nusu saa pekee. Nyuso za watazamaji ziling’ara kwa furaha tele huku zile za waafrika ambao walikuwa wanaelewa kiswahili zikabaki meno nje kwa kucheka na kutafakari maneno yaliyokuwa yanaimbwa.
Tulifika pale karibu dakika thelathini kabla ya kuanza kwa onyesho. Jamaa walikuwa wanang’ang’ania tikiti ili wamudu kuwaona hawa wana Culture Music Club kutoka Tanzania ambao wamesifika dunia nzima kwa muziki wao uliochangamka na uzoefu mkubwa ambao unaunganisha bara Asia, Afrika na tamaduni za uarabuni. Mbali na Afrika, sifa zao nyingi hasa zajulikana Ulaya ambako wameweza kutembelea nchi nyingi mara kwa mara wakitumbuiza kwa muziki wao. Kikundi hiki kimerekodi kazi zake nyingi Ulaya. Ingawa watu wa bara la ulaya wamepata kununua kazi zao, na kuwaona mara kadhaa jukwaani, ni vigumu kwa mtu kujizuia kuwaona tena na tena kwani maonyesho yao hayaishi hamu. Kwetu sisi, hii ilikuwa mara yetu ya kwanza kujumuika na watu wa ulaya kwenye onyesho hili la muziki ambapo uliwakilisha tamaduni ya mwambao vizuri.
Wakati tunaingia kwenye ukumbi wa Centralstation dakika chache kabla ya kuanza kwa onyesho, watu tayari walikuwa wametapakaa kote huku wakiongeleshana na kujuliana hali huku wakijituliza kwa vinywaji. Jukwaa lilikuwa limejaa vipaza sauti tofauti tofauti ili kuwezesha sauti kusikika vizuri katika ukumbi wote. Lakini hakukuwa na ala hata moja ya muziki jukwaani.
Punde, taa zikapunguzwa huku nyingine zikizimwa kabisa na kuacha mwangaza katika jukwaa peke yake, hali iliyoonyesha kwamba wakati ulikuwa umewadia. Watazamaji wakaharakisha kutafuta mahali pa kukaa huku wengine wakiandaa kamera ili kuchukua picha. Mara tukasikia makofi ya kushangilia huku wenye vyombo vya kuchukuwa picha wakitafuta nafasi bora ya kupiga picha za wanamuziki. Wasanii wakajipanga kwenye jukwaa huku kila mmoja ameshikilia ala yake ya muziki. Mbele ya jukwaa walijipanga wanaume ambao walivalia kanzu nyeupe na kofia za watu wa mwambao huku wakiongeza na koti jeusi juu. Wanawake waliojipanga kwa kukaa katika mstari wa nyuma nao walikuwa wavalia mavazi yao ya kupendeza ya hariri iliyong’ara kwa kumulikwa na taa. Kwa mavazi yao na mpangilio wao, hawa wana Culture Music Club waashiria uvaaji unaopendelewa na watu wa mwambao. Kwa ujumla kulikuwa na wanawake watatu, wawili wanaimba solo na mmoja wao ambaye alicheza dufu.
Kwa ujumla, kulikuwa na wanaume tisa na wanawake watatu ambao walikaa kwa mpangilio huu;
Chorus (mwanamke)
Chorus (mwanamke)
Chorus na Rika/Dufu (mwanamke)
Akodion (mwanamme)
Dumbak (mwanamme)
Bongos (mwanamme)
Ud (mwanamme)
Zeze/Violin (mwanamme)
Zeze/Violin (mwanamme)
Zeze/Violin (mwanamme)
besi maradufu/Double Bass (mwanamme)
Qanun (mwanamme)
Wakati wa kuimba, mwimbaji alikuwa anasogelea mbele kabisa ya jukwaa. Majina ya hawa wanamuziki ni kama ifuatavyo;
Rajab Suleiman Ambaye alicheza qanun mara ya kwanza, na halafu kidumbak kwa onyesho la kipindi cha pili. Mwanamme wa pili ni Ali Hassan ambaye naye ni chezaji wa ‘ud, na pia cherewa ambayo ilikuwa kwa onyesho la kipindi cha pili. Ramadhani Khamis na Kesi Juma wote wawili walicheza zeze. Naye Makame Faki alicheza zeze na pia akaongoza kikundi katika kuimba nyimbo kadhaa. Taimur Rukun alicheza akodion, halafu baadaye akacheza mkwasa sehemu ya pili ya onyesho. Pia alisemekana kuwa ndiye kiongozi wa kikundi hiki cha wana Culture Music Club. Mahmoud Juma naye ni mchezaji wa besi maradufu ama kwa kiingereza, double bass. Foum Fakialikuwa kwa ngoma za bongos na pia kidumbak kwa sehemu ya pili, halafu mwishowe akawa ni Amour Haj ambaye alicheza dumbak, na kisha baadaye akamalizia na sanduku kwa sehemu ya pili. Kwa upande wa wanawake kulikuwa na Rukia Ramadhani ambaye aliongoza waimbaji na wachezaji kwa kuimba nyimbo kadhaa. Wa pili akawa Mgeni Khamis ambaye aliongoza wengine kwa kuimba, kisha akacheza dansi na kuimba kwa sehemu ya pili ya onyesho. Mwishowe kukawa na Fatma Juma ambaye alikuwa muimbaji huku akicheza rika. Baadaye kwa sehemu ya pili akaimba na kucheza dansi ya kusisimua sana.
Baada ya kupigiwa makofi ya kuwashangila, wote waliinama kusalimia na kupokea salamu, kisha wakakaa ila mpiga besi maradufu akabaki amesimama. Mara mmoja wa wale wapiga zeze/fidla akainua mkono wake ulioshikilia upinde wa zeze/fidla, na kuashiria “tayari tuanze”. Muziki wa ala ukapigwa taratibu huku ukijikita kwenye maudhui tofauti tofauti kwa karibu ya dakika nane mfululizo. Wakati huu kila chombo kiliweza kupata nafasi ya kuweza kusikika kwa kupewa msisitizo kwa muda. Kama ilivyo desturi ya baadhi ya miziki mingi yenye asili ya Afrika, sehemu hii ilitia kikomo bila watu kutarajia. Kuisha huku kwa kushtukiza, pengine ni kwa sababu ya utamu uliozidi kukolea kadiri walivyoendelea kucheza ala hizo. Makofi yakabubujika kutoka kwa watazamaji huku jamaa wangu wa kucheza besi maradufu akishukuru kwa kupeperusha mabusu kedekede.
Kikundi hiki cha Culture kimeonekana kuwa mahiri sana hasa katika matumizi ya jukwaa. Muda wote wamejitahidi kuhakikisha wanatumia jukwaa lote kwa ukamilifu wake huku watazamaji wakipata nafasi sawa ya kuona kila kinachoendelea jukwaani. Ingawa mfumo wa wasanii wanawake kujipanga nyuma ya jukwaa ndio mfumo wa taarab asili, bado nafasi na mvuto wao ulikuwa sawa au hata zaidi ya wasanii waliojipanga katikati au hata mbele ya jukwaa.
Ili kuweza kufahamu ni kwa jinsi gani wameweza kuwa wataalamu wa kutumia jukwaa kwa ustadi huo, wasanii wa Culture walikiri wazi kuwa wamekuwa wakipata mafunzo mbalimbali na ya mara kwa mara katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo (Bagamoyo College of Arts). Hii imewasaidia kuweza kufanya kazi yao kwa ufanisi na ubunifu zaidi na hata pia katika kuimba na kupiga ala.
Sehemu ya pili ikaanza kwa utaratibu. Wakati huu makofi ya kushangilia sehemu ya kwanza yalikuwa yameshatulia. Basi akaamka mwanaume mwenye umri wa karibu miaka sitini hapo akasogelea kipaza sauti. Tukasikia makofi tena ya kumshangilia. Baada ya kusikiliza na kuyatafakari yale makofi tulipata kuelewa ya kwamba labda baadhi ya wengi wa wasikilizaji kwenye ukumbi walikuwa wanamfahamu huyo mzee. Huyu alikuwa mzee Makame Faki. Sauti yake yenye tajiriba nyingi ilivuma kwenye ukumbi wote huku akililia mpenzi wake arudi; kwamba atampokea.
Baada ya Bwana Faki kuwaloga watu na wimbo wake wa ‘Njoo’, wimbo ambao aliuvumisha kwa sauti yake mwanana ya kuliwaza mwana, mmoja wa wale wanamuziki wa kike aliamka kwa maringo kama tausi na mavazi yenye kupendeza sana. Akachukuwa nafasi yake mbele na kuwaonyesha waliokuwa kwenye ukumbi kwamba taarab ni ya wake kwa waume. Kitu cha kushangaza ni vile alivyokuwa na sauti yenye upeo mkubwa. Aliweza kuimba soprano kama ya chiriku halafu baadaye tena akaweza kuimba hata kuikaribia ile sauti nzito ya bwana Faki.
Yule mwanamuziki wa kike wa pili naye alipotokea ikaonekana atashinda wote waliokuwa wamemtangulia. Ubora wake hasa ulikita kwenye maneno ambayo aliweza kuyatamka yakaeleweka vyema kwa sauti yake nyororo. Uso wake uling’ara kwa kutafakari maneno yale alipokuwa anaimba. Hivi aliweza kuwavutia watazamaji ambao baadhi yao walimtuza kwa manoti.
Baada ya kutumbuiza kwa nyimbo sita, kukawa na sehemu ya mapumziko ambapo watu waliweza kukamata chupa ya maji au kahawa na vinywaji vingine vingi huku wakiongea sifa za wanamuziki hawa. Baada ya mapumziko kulikuwa na sehemu ya muziki wa ala ambao ulitumiwa kuwaanda watu kwa onyesho la kukata na shoka. Bwana Faki alifuatia na wimbo wake ulioelezea vile alivokuwa dhahabu siku zake zilizopita kwa mpenzi wake na hata familia. Wimbo huu ulivutia wengi ambao walimtunuku kwa pesa huku wakicheza kuonyesha furaha.
Ili kufungasha virago kwa kuacha alama ya kukumbukwa milele, walifanya mabadiliko kwenye mpangilio wa jukwaa. Wanamuziki wa kike walikwenda kubadilisha mavazi kwa kuvaa yale ya kuwawezesha kucheza. Sehemu hii yenye muziki wa dansi inajulikana kama ‘kidumbak’. Ala nyingi zilipata kubadilishwa kama vile besi maradufu ambayo ikabadilishwa na sanduku ambayo ni gitaa kubwa yenye ukanda mmoja na ya asili ya kiafrika toka Tanzania kaskazini. Kulikuwa pia na cherewa au manyanga (shakers) na mkwasa (claves). Kulibaki na zeze/fidla (violin) mbili na Ki-Ndumbak (ngoma zenye asili ya Kihindi) mbili. Wachezaji wote waliweza pia kuimba.
Sehemu hii ilipamba moto huku waimbaji na wachezaji wakichamgamka na kuchangamsha umati ikaonekana kana kwamba walikuwa wanangoja sehemu hii. Bwana Faki ambaye alikuwa mwimbaji, alicheza na ikawa vigumu kwa mtu kuamini alikuwa na umri wa miaka sitini na tatu. Wengi wa watu kwenye umati waliungana nao kwa kucheza, ukumbi ukabadilika kuwa disko. Ilipofika tamati ya onyesho lao, watu walishangilia kwa makofi na vigelegele mpaka ikabidi warudie kuimba tena angalao wimbo mmoja.
Kama kawaida ya nyimbo za taarab waimbaji walitilia mkazo maelezo ya mapenzi kati ya wale wapendanao. Sifa zilibubujika pale mapenzi yanaponawiri huku wapendanao wakiagiza kuyaboresha zaidi. Kwenye nyimbo hizi pia mafunzo tele tele kuhusu uhusiano kati ya mume na mke yaliweza kuchambuliwa na kufafanuliwa. Uchungu wa kukosana na juhudi za kutaka kurudiana baada ya mambo kwenda mrama, ni baadhi ya yale yaliyowekewa msisitizo.
Bendi hii ya Culture Music Club ilianzishwa mwaka wa 1958 na hadi sasa imeshakuwa na wasanii takribani 60 wanaoimba na kucheza vyombo na ala nyingine za muziki. Wasanii hawa ni mchangnyiko wa vijana na wazee, ishara kwamba kuna watu wa kurithi na kuiendeleza bendi hiyo kimuziki kwa miaka mingi ijayo. Kitu kinachojitambulisha kwa hawa wana Culture Music Club ni vile wanavyochanganya tamaduni mbalimbali ndani ya muziki wanaopiga. Kwanza kabisa ni kwamba kuna mchanganyiko wa sauti ambazo zinajumulisha hisia za Uarabuni, bara Asia na Afrika. Tamaduni zingine zaonyeshwa na mkusanyiko wa vyombo vya muziki ambavyo ni vya asili ya sehemu mbali mbali kama vile Misri, Ulaya, Uarabuni, India na nyinginezo kutoka Afrika. Kwa mfano Qanun ni Zither yenye asili ya Uarabuni, zeze na besi maradufu nazo zikaunganisha bara Asia na Ulaya. Sanduku, cherewa, na hata mkwasa ni baadhi ya zile zenye asili ya Kiafrika.
Muziki wenyewe nao uliweza kuumbwa kwa kuchanganya aina mbalimbali ya midundo. Kwa mfano kuna vile niweza kusikia mdundo wa ‘rhumba’, ukafuatiwa na ‘lingala’, ‘cha cha cha’ nk. Mahadhi yaliyo katika mpangilio wa 12/8 yaliweza kutambulika pia. Haya ni mahadhi yenye asili ya muziki wa Afrika. Wakati mwingine zeze ilipigwa kufuata mfumo wa gitaa za wanamuziki toka Kongo na hata Tanzania kwenyewe wanakotoka hao wana Culture Music Club. Mengi ya mafunzo yanayogusiwa katika nyimbo zao yanatokana na yale ambayo yanatendeka mara kwa mara katika jamii wanamotoka baadhi ya wale wanamuziki. Kwa kawaida ya wanamuziki wa asili ya Afrika inakuwa jukumu lao sio tu kuwatumbuiza bali pia kuwaelimisha wanaosikiliza muziki huo. Nafasi wanayopata kupitia muziki ndio nafasi ya kupashana habari na kujumuika na watu mbali mbali kama jamii moja.
Mwanzo kucheza Kidumbak kwenye muziki wa taarab ilikuwa nadra. Lakini kwa sasa inaonekana kuibua hisia za upya na maendeleo. Baadhi ya ufafanuzi ni kwamba wanajaribu kuufanya muziki huu uweze kuwavutia wengi wa waafrika kwa kujikita kwenye mizizi ya tamaduni za Kiafrika. Taarab ni aina ya muziki ambao imejulikana kwa kujaribu kuleta tamaduni tofauti pamoja. Hivyo basi, taarab inachangia kwa kiasi kikubwa hali hii ya ‘utandawazi’ kwa kuchanganya tamaduni mbalimbali. Umri mkubwa wa baadhi ya wanamziki unaonyesha uzoefu sio tu kwa kucheza na kuimba, bali pia kwa kupanga yale wanayoimba ili kusaidia kukuza maadili na mafunzo mengine katika jamii.
Mpunga ni mojawapo ya nyimbo walizocheza hawa wana Culture Music Club.
Moja ya nyimbo za Culture Music Club kutoka Zanzibar, Tanzania
Transcribed and translated by Aggrey Nganyi Wetaba and Vicensia Shule on 20.11.2007
Mpunga
Verse 1
| Mwendo mbaya huachi Mbinu ni kutanga tanga Tena wala Hujifichi Ukiuona mpunga Waingia kwenye nichi Wala hujui kutwanga | You don’t give up your bad ways Your ways of roaming about You don’t even hide Whenever you see unhusked rice You get into the mortar And yet you don’t know how to pound! |
Chorus
| Akili zako ni changa Mambo unayavuruga Wala hujui kutwanga Mpunga unaumwaga | Your brains are still young You mess up issues Yet again you don’t know how to pound You spill the rice |
Verse 2
| Oho ulijitia usugu Miti mingi ukachonga Oho kumbe vile ni vurugu Akili zako ni changa Umezama kwenye uchungu Hegali ndege watunga | Oho, you make your life difficult Curving many pestles (sticks) Oho but it is just disturbance Your brains are young You have sunk into pain Even birds fly away |
Chorus
| Akili zako ni changa Mambo unayavuruga Wala hujui kutwanga Mpunga unaumwaga | Your brains are still young You mess up issues Yet again you don’t know how to pound You spill the rice |
Verse 3
| Oho kwa watu wasema nini? Dunia imekuzonga Oho mambo yako kweupeni Sasa unamanga manga Tenje yako ya debeni Imeingia mchanga | Oho, what are you telling people now? The world is closing down on you Your issues are now in public Now you are roaming about Your Tenje system of 20lt container type Has been soiled! |
Chorus
| Akili zako ni changa Mambo unayavuruga Wala hujui kutwanga Mpunga unaumwaga | Your brains are still young You mess up issues Yet again you don’t know how to pound You spill the rice |
