| Article Index |
|---|
| Culture Music Club in Darmstadt |
| Page 2 |
| Page 3 |
| Page 4 |
| Page 5 |
| All Pages |
Ili kuweza kufahamu ni kwa jinsi gani wameweza kuwa wataalamu wa kutumia jukwaa kwa ustadi huo, wasanii wa Culture walikiri wazi kuwa wamekuwa wakipata mafunzo mbalimbali na ya mara kwa mara katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo (Bagamoyo College of Arts). Hii imewasaidia kuweza kufanya kazi yao kwa ufanisi na ubunifu zaidi na hata pia katika kuimba na kupiga ala.
Sehemu ya pili ikaanza kwa utaratibu. Wakati huu makofi ya kushangilia sehemu ya kwanza yalikuwa yameshatulia. Basi akaamka mwanaume mwenye umri wa karibu miaka sitini hapo akasogelea kipaza sauti. Tukasikia makofi tena ya kumshangilia. Baada ya kusikiliza na kuyatafakari yale makofi tulipata kuelewa ya kwamba labda baadhi ya wengi wa wasikilizaji kwenye ukumbi walikuwa wanamfahamu huyo mzee. Huyu alikuwa mzee Makame Faki. Sauti yake yenye tajiriba nyingi ilivuma kwenye ukumbi wote huku akililia mpenzi wake arudi; kwamba atampokea.
Baada ya Bwana Faki kuwaloga watu na wimbo wake wa ‘Njoo’, wimbo ambao aliuvumisha kwa sauti yake mwanana ya kuliwaza mwana, mmoja wa wale wanamuziki wa kike aliamka kwa maringo kama tausi na mavazi yenye kupendeza sana. Akachukuwa nafasi yake mbele na kuwaonyesha waliokuwa kwenye ukumbi kwamba taarab ni ya wake kwa waume. Kitu cha kushangaza ni vile alivyokuwa na sauti yenye upeo mkubwa. Aliweza kuimba soprano kama ya chiriku halafu baadaye tena akaweza kuimba hata kuikaribia ile sauti nzito ya bwana Faki.
Yule mwanamuziki wa kike wa pili naye alipotokea ikaonekana atashinda wote waliokuwa wamemtangulia. Ubora wake hasa ulikita kwenye maneno ambayo aliweza kuyatamka yakaeleweka vyema kwa sauti yake nyororo. Uso wake uling’ara kwa kutafakari maneno yale alipokuwa anaimba. Hivi aliweza kuwavutia watazamaji ambao baadhi yao walimtuza kwa manoti.
Baada ya kutumbuiza kwa nyimbo sita, kukawa na sehemu ya mapumziko ambapo watu waliweza kukamata chupa ya maji au kahawa na vinywaji vingine vingi huku wakiongea sifa za wanamuziki hawa. Baada ya mapumziko kulikuwa na sehemu ya muziki wa ala ambao ulitumiwa kuwaanda watu kwa onyesho la kukata na shoka. Bwana Faki alifuatia na wimbo wake ulioelezea vile alivokuwa dhahabu siku zake zilizopita kwa mpenzi wake na hata familia. Wimbo huu ulivutia wengi ambao walimtunuku kwa pesa huku wakicheza kuonyesha furaha.
