| Article Index |
|---|
| Culture Music Club in Darmstadt |
| Page 2 |
| Page 3 |
| Page 4 |
| Page 5 |
| All Pages |
Kwa ujumla, kulikuwa na wanaume tisa na wanawake watatu ambao walikaa kwa mpangilio huu;
Chorus (mwanamke)
Chorus (mwanamke)
Chorus na Rika/Dufu (mwanamke)
Akodion (mwanamme)
Dumbak (mwanamme)
Bongos (mwanamme)
Ud (mwanamme)
Zeze/Violin (mwanamme)
Zeze/Violin (mwanamme)
Zeze/Violin (mwanamme)
besi maradufu/Double Bass (mwanamme)
Qanun (mwanamme)
Wakati wa kuimba, mwimbaji alikuwa anasogelea mbele kabisa ya jukwaa. Majina ya hawa wanamuziki ni kama ifuatavyo;
Rajab Suleiman Ambaye alicheza qanun mara ya kwanza, na halafu kidumbak kwa onyesho la kipindi cha pili. Mwanamme wa pili ni Ali Hassan ambaye naye ni chezaji wa ‘ud, na pia cherewa ambayo ilikuwa kwa onyesho la kipindi cha pili. Ramadhani Khamis na Kesi Juma wote wawili walicheza zeze. Naye Makame Faki alicheza zeze na pia akaongoza kikundi katika kuimba nyimbo kadhaa. Taimur Rukun alicheza akodion, halafu baadaye akacheza mkwasa sehemu ya pili ya onyesho. Pia alisemekana kuwa ndiye kiongozi wa kikundi hiki cha wana Culture Music Club. Mahmoud Juma naye ni mchezaji wa besi maradufu ama kwa kiingereza, double bass. Foum Fakialikuwa kwa ngoma za bongos na pia kidumbak kwa sehemu ya pili, halafu mwishowe akawa ni Amour Haj ambaye alicheza dumbak, na kisha baadaye akamalizia na sanduku kwa sehemu ya pili. Kwa upande wa wanawake kulikuwa na Rukia Ramadhani ambaye aliongoza waimbaji na wachezaji kwa kuimba nyimbo kadhaa. Wa pili akawa Mgeni Khamis ambaye aliongoza wengine kwa kuimba, kisha akacheza dansi na kuimba kwa sehemu ya pili ya onyesho. Mwishowe kukawa na Fatma Juma ambaye alikuwa muimbaji huku akicheza rika. Baadaye kwa sehemu ya pili akaimba na kucheza dansi ya kusisimua sana.
Baada ya kupigiwa makofi ya kuwashangila, wote waliinama kusalimia na kupokea salamu, kisha wakakaa ila mpiga besi maradufu akabaki amesimama. Mara mmoja wa wale wapiga zeze/fidla akainua mkono wake ulioshikilia upinde wa zeze/fidla, na kuashiria “tayari tuanze”. Muziki wa ala ukapigwa taratibu huku ukijikita kwenye maudhui tofauti tofauti kwa karibu ya dakika nane mfululizo. Wakati huu kila chombo kiliweza kupata nafasi ya kuweza kusikika kwa kupewa msisitizo kwa muda. Kama ilivyo desturi ya baadhi ya miziki mingi yenye asili ya Afrika, sehemu hii ilitia kikomo bila watu kutarajia. Kuisha huku kwa kushtukiza, pengine ni kwa sababu ya utamu uliozidi kukolea kadiri walivyoendelea kucheza ala hizo. Makofi yakabubujika kutoka kwa watazamaji huku jamaa wangu wa kucheza besi maradufu akishukuru kwa kupeperusha mabusu kedekede.
Kikundi hiki cha Culture kimeonekana kuwa mahiri sana hasa katika matumizi ya jukwaa. Muda wote wamejitahidi kuhakikisha wanatumia jukwaa lote kwa ukamilifu wake huku watazamaji wakipata nafasi sawa ya kuona kila kinachoendelea jukwaani. Ingawa mfumo wa wasanii wanawake kujipanga nyuma ya jukwaa ndio mfumo wa taarab asili, bado nafasi na mvuto wao ulikuwa sawa au hata zaidi ya wasanii waliojipanga katikati au hata mbele ya jukwaa.
